Katika maeneo mengi ya Afrika, udongo umechoka, umeshindiliwa, miti imekatwa. Kwa sababu hiyo, maji ya mvua hayanyonyeshwi tena udongo, bali hutiririka bila kudhibitiwa, na kusomba udongo wa juu wenye rutuba na hata kusababisha mafuriko mahali pengine ambayo yanaweza kugharimu maisha.
Kuna nyasi moja ambayo inaweza kusaidia kutatua tatizo hili: Mkasikasi au Mzumai (Chrysopogon zizanioides). Mizizi yake hufikia kina kirefu ardhini (hadi mita nne). Hii huifanya nyasi kustahimili ukame, hivyo kusaidia kuingiza hewa kwenye udongo na kuruhusu maji mengi ya mvua kupenya kwenye udongo. Tabia yake ya ukuaji thabiti na mizizi ya kina pia huzuia nyasi kubebwa na maji. Kazi ambazo "nyasi ya miujiza" inaweza kufanikisha ni nyingi:
- Kama udhibiti wa mmomonyoko wa ardhi, ili kuzuia mvua isibebe udongo. Inaweza hata kupandwa katika korongo kubwa za mmomonyoko. Au mikasikasi hupandwa kwenye mistari ya kontua kwa ajili ya kuzuia mmonyoko usianze, bali maji yapenye ardhi.
- Kando ya njia na pembeni kwa mashamba kama alama. Kwa sababu ina mizizi mirefu na haina tabia ya kutambaa, inakaa mahali pamoja kwa miaka mingi. Pia inaonekana vizuri.
- Kama matandazo kwa shamba. Mkasikasi huendelea kuota hata wakati wa kiangazi na ni nzuri sana kwa matandazo ya mashambani, kwenye mboga mboga au miti iliyopandwa.
- Ikipandwa kama duara kubwa kuzunguka migomba, inafaa kama nyenzo ya matandazo na pia kuzuia mvua kubwa kusomba matandazo.
- Kama sehemu ya mbinu jumuishi ya kudhibiti wadudu. Baadhi ya wadudu wa nafaka wanapendelea mkasikasi na hivyo basi kuacha mazao ya nafaka kama vile mahindi. Hata hivyo, hawawezi kuzaliana kwenye nyasi ya mkasimkasi, hivyo shinikizo la wadudu kwa ujumla hupunguzwa.
- Kama hifadhi ya malisho kwa msimu wa kiangazi. Kwa kuwa huendelea kuchipua, wanyama wana akiba wakati malisho meingine hayapatikani tena.
- Mizizi ina mafuta muhimu ambayo hutumiwa katika tasnia ya pafum.
- Na watu wanapata matumizi mengine zaidi kila wakati!
Yote kwa yote, ni nyasi ya ajabu yenye kazi nyingi ambayo sisi hutumia kwa njia nyingi kwenye shamba letu. Miaka minne iliyopita tulianza na fungu moja la nyasi na sasa tuna mamia yao katika shamba letu. Mfano mwingine wa uwezo wa kurejesha ambao Mungu ameweka katika uumbaji wetu!