Tunapenda kumshukulu Mungu kwa mvua ambazo zimenyesha kifuku na mpaka sasa tunajiandaa na kazi za kipindi cha kiangazi. Kazi zetu kubwa sana msimu wa kiangazi mara nyingi ni umwagiliaji wa miti midogo hasa hasa ya matunda, umwagiliaji wa viploti vya maonyesho kwa ajili ya kuonyesha mbinu mbalimbali za kilimo kipindi cha semina. Kwa mwaka huu tunatazamia kupata kiangazi kikubwa kwa sababu mvua zilichelewa kunyesha - zimeanza mwezi wa pili - na zimekatika mapema. Kwa kawaida hapa Dodoma mvua huwa zinawahi kunyesha huanza mwezi 11 au 12, na inanyesha milimita 500 kwa mwaka. Lakini mwaka huu imenyesha tu kama milimita 350, kwa hiyo maji yaliyoingia ardhini ni machache, na hivyo basi tutakuwa na kazi kubwa ya kumwagilia. Pamoja na kazi ya umwagiliaji tunakuwa na kazi ya kukusanya blanketi ya Mungu (matandazo ya majani) na kila mwenye eneo anaweka kwenye miti na kuhifadhi nyingine kwa ajili ya msimu wa mvua kwa sababu pale kunakuwa na upandaji mkubwa.
Kazi nyingine ni maandalizi mengine kwa mvua ijayo, kama kuongeza na kurefusha mabwawa, kilimo cha mbogamboga, mavuno ya mbaazi na mihogo, na kuchunga mifugo yetu. Hizi ndizo kazi zetu kubwa kipindi cha kiangazi kwenye mashamba yetu...